Wednesday, April 30, 2008

JACKSON A.K.A 50 CENT,



Mwanamuziki nyota wa Hip Hop toka nchini Marekani, Curtis Jackson maarufu kama ‘50 Cent’ atamtambulisha mwanachama mpya wa kundi la G-unit katika onyesho lake la Jumapili litakalofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Meneja Masoko wa kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Kelvin Twissa ambayo ndio inamleta 50 Cent na kundi zima la G-Unit, msanii huyo mpya aliyejiunga na kundi hilo hivi karibuni atatambulishwa kwenye onyesho la Diamond kama bonasi kwa wapenzi wao.

Baadhi ya wasanii wa G-Unit ambao kirefu chake ni Guerrilla Unit watakaofika hapa nchini, mbali na 50 Cent wengine ni Lloyd Banks , Tony Yayo na mwanadada Olivia. Kundi hilo kwa sasa lina albamu mpya inayojulikana kama ‘Terminate on Sight’ ikiwa ni albamu yao ya pili tokea kundi hilo kuanzishwa 2002.

50 Cent na G-Unit watawasili siku hiyo ya onyesho na kufanya onyesho hilo linalosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa muziki wa hip hop wa Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani. Twissa alisema tayari Tigo imekwishatoa tiketi 400 kwa wateja wake kwa ajili ya kwenda kushuhudia onyesho hilo na kuwa tiketi nyingine 300 zitatolewa keshokutwa kwa wateja ambao watashinda katika promosheni inayoendelea kwa ajili ya onyesho la nyota huyo.

“Tunajua watu wengi wanatamani sana kumshuhudia nyota huyo, tunawaomba waendelee kutuma ujumbe wenye neno Muziki ili kujishindia tiketi,” alisema. Kwa mashabiki na wapenzi wengine wa muziki wa 50 Cent ambao hawatashinda tiketi kwenye promosheni hizo wanaweza kununua tiketi kwa Sh 50,000 , 30,000 na kwa wale watakaonunua tiketi zao mlangoni watatakiwa kulipa Sh 40,000.

Source: Habari Leo 2 bongo5.com

No comments: